Kaimu mwenyekiti wa klabu ya Yanga Sc tawi la bungeni ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Chalinze Mh. Ridhiwan Kikwete ametangaza kuwania nia ya kuwekeza ndani ya klabu ya Yanga Sc.
Akizungumza na kipindi cha michezo na burudani cha redio Free Afrika Ridhiwan amesema lengo lake kubwa ni kuhakikisha Yanga inaondokana na tatizo la ukata wa fedha ili kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi kuu na ya kimataifa.
“Mimi nafsi yangu katika jambo ambalo huwa nalipigania sana ni kuutaka uongozi wa Yanga Sc ubadilishe mfumo wa uendashaji wa klabu yetu na ni ukweli itakapofika hatua hiyo na mimi niweze kutafuta vijisenti kidogo ili tuingize kuisaidia klabu yetu.
Mimi ni mmoja kati ya watu ambao wanatamani sana kuona Yanga Sc ikiongozwa katika mfumo wa kisasa, kwasababu mfumo uliopo sasaivi ndiyo umetufanya kuwa kwenye hali hii mpaka sasa ya kutangatanga.
Tupo tayari kuwekeza ndani ya klabu ya Yanga tena sana, Simba wameamua kuwa thamani ya klabu yao ni bil. 20 lakini mimi siamini kama Yanga thamani yao ni bil. 20, thamani ya Yanga ni zaidi ya bil. 20
Binafsi naiheshimu sana Simba na naheshimu sana viongozi wa Simba lakini kwangu mimi naona kabisa wameuza hisa zao kwa bei rahisi sana, kwa klabu kubwa kama Simba Sc, historia yake na heshima yake ndani ya nchini hii na kusema Simba ina thamani hiyo mimi kwangu hapana.
Wanayanga wanahitaji sana utulivu katika kipindi hiki na wasife moyo kwasababu klabu hii ipo mikononi mwao bado na wao ndiyo wanaoweza kuamua.
Lakini pia nawaomba sana mashabiki wa Yanga wasiwe wenye kuropoka, wasitishwe na mafanikio ya hivi vikao vya siku 2 vya Simba”
Hayo yalikuwa ni maneno aliyotamka Ridhiwani Kikwete alipokuwa akifanya mahojiano na kipindi cha Michezo na Burudani kinachorushwa na Redio Free Afrika.
Ikumbukwe Yanga Sc inatarajia kufanya mkutano wake siku ya Jumapili tar 10 June 2018 ili kujadili mchakato huo wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.