Yusuph Mhilu kwa sasa ndiye nyota wa safu ya ushambuliaji ya kikosi cha Yanga. Bila shaka ndiye anayebeba matarajio ya wengi kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Wolaitta Dicha nchini Ethiopia.
Ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Yanga kwenye uwanja wa Taifa katika mchezo wa kwanza ulichangiwa kwa asilimia 80 na chipukizi huyo aliyepandishwa kikosi cha kwanza na kocha wa zamani wa Yanga Hans van Pluijm misimu miwili iliyopita.
Pasi yake murua kwa Haji Mwinyi kwenye sekunde ya 28 ilizaa bao la kuongoza lililofungwa na Raphael Daudi Lothi aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Mwinyi.
Mhilu pia ndiye aliyejaza majaro iliyowekwa kimiani na Emanuel Martin kuihakikishia Yanga ushindi muhimu nyumbani.
Yanga inahitaji sare au ushindi ugenini kujihakikishia kutinga hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.
Ni dakika tisini tu zilizosalia, Jumatano ijayo huko Hawassa kitaeleweka.