VPL: Azam, MCC wagawana pointi, Njombe wakiadabishwa na Stand
Mzunguko wa 23 wa ligi kuu soka Tanzania umeendelea Jumapili ya April 8, 2018 kwa michezo minne iliyopigwa katika viwanja vya miji ya Mtwara, Mbeya, Shinyanga na Mlandizi kule mkoani Pwani.
Katika mchezo mkali uliofanyika kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, wageni timu ya soka ya Azam FC 'Wanalambalamba' wameilazimisha sare ya bila kufungana timu ya soka ya Mbeya City 'Wanakomakumwanya'.
Mchezo huo ulikuwa mkali na kila timu ikijaribu kushambulia kwa kasi lakini hadi mwisho hakuna timu yoyote iliyopata bao, na kuishia kugawana alama zinazowafanya kila timu kuambulia alama moja na kuwa mtaji kwenye hatua ya hii ya lala salama.
Stand 3-1 Njombe
Mkoani Shinyanga katika uwanja wa CCM Kambarage, Stand United 'Chama la Wana' wameendeleza ubabe mbele ya timu ya soka ya Njombe Mji baada ya kuwachapa kwa mabao 3-1.
Stand United walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya kwanza tu ya Mchezo kupitia kwa Seleman Ndikumana baada ya kuonganisha krosi ya Tariq Seif, huku mabao mengine mawili yakifungwa na Sixtus Sabilo katika dakika ya 84 na 90 ya mchezo huo, bao pekee la Njombe Mji limefungwa na Notkelly Masasi katika dakika ya 75.
Ndanda 1-1 Kagera
Katika uwanja Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, 'Wanakuchele' Ndanda FC wamelazimisha sare ya bao 1-1 na wanankurukumbi Kagera Sugar.
Kagera Sugar wamepata bao lao kupitia kwa Abdallah Mguhi katika dakika ya 27 kabla ya Mrisho Khalifan Ngassa kusawazisha katika dakika ya 33 ya mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani kutoka pande zote mbili.
Mchezo wa mwisho umewakutanisha Wafunga buti Ruvu Shooting na wajelajela Tanzania Prisons, na kushuhudia timu hizo zikigawana pointi baada ya kutoka suluhu ya 0-0 mchezo ambao umefanyika katika uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.