Na Mwandishi Wetu, ALGER
WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva usiku huu amecheza kwa dakika 87, timu yake Difaa Hassan El-Jadida ikilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Mouloudia Club D'Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers.
Msuva ambaye yupo katika msimu wake wa kwanza tu Difaa Hassan El- Jadidi tangu ajiunge nayo Juni mwaka jana kutoka kwa mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Yanga SC, alimpisha kiungo Mmorocco, Houssine Khoukhouche kumalizia dakika tatu za mwisho.
Na wakati anaondoka uwanjani Msuva ambaye timu yake imepangwa Kundi B pamoja na Mouloudia Club D'Alger, E. S. Setifienne ya Algeria na TP Mazembe ya DRC tayari ilikuwa imekwishafungana 1-1 na MC Alger.
Na walikuwa ni wageni, Difaa Hassan El-Jadidi waliotangulia kwa bao la mshambuliaji Mmorocco mwenye umri wa miaka 23, Hamid Ahadad dakika ya 77, kabla ya Amir Karaoui kuwasawazishia wenyeji, MC Alger dakika ya 82.
Mechi nyingine za leo za ufunguzi hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly imelazimishwa sare ya 0 – 0 na ES Tunis Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria mna bao pekee la Lemponye Tshireletso dakika ya 36 limetosha kuipa ushindi wa 1-0 Township Rollers dhidi ya KCCA ya Uganda Uwanja wa Taifa wa Gaborone nchini Botswana.