HOUSE OF ENTERTAINMENT


JOIN KENYASWAHILINEWS
!-- AdsAgony - Ad Display Code -->

MPYA MPYA ZA LEO

HABARI (193) Michezo (121) BURUDANI (86)

Jumamosi, 5 Mei 2018

PLUIJM KIZA KINENE AZAM


NA SAADA SALIM |

IMEBAINIKA itakuwa ngumu kwa Kocha Mkuu wa Singida United, Hans van der Pluijm, kujiunga na kikosi cha Azam, baada ya timu yake hiyo ya mkoani Singida kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (Azam Confederation Cup).

Hali hiyo imezua hofu kwa uongozi wa Azam kwani endapo Singida United watafanikiwa kushinda kombe hilo, watakuwa wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo haitakuwa rahisi kwa Pluijm kuondoka.

Hofu hiyo imekuja baada ya Azam kuamini Singida United wanaweza kumzuia Mholanzi huyo ili awaongoze katika michuano hiyo ya kimataifa kutokana na uzoefu wake, akiwa ameshawahi kukiongoza kikosi cha Yanga.

Habari za ndani kutoka kwa watu walio karibu na Pluijm, zinasema kuwa kocha huyo amesaini mkataba wa miaka miwili wa kukinoa kikosi cha Azam, kuanzia msimu ujao akichukua nafasi ya Aristica Cioaba.

Akizungumza na BINGWA Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Azam, Idrissa Nassor ‘Father’, alikataa klabu yao kuingia mkataba na Pluijm, wakiamini bado ana mkataba na Singida United.

“Pluijm hatuwezi kumchukua kwa sababu yupo Singida United ambayo imeingia fainali ya Kombe la Azam, endapo wakishinda kombe hilo, nina hakika tutakuwa na wakati mgumu wa kumpata sababu watamuhitaji kocha huyo mzoefu katika michuano ya kimataifa.

Juu ya taarifa kuwa Cioaba ameondoka moja kwa moja, Father alikanusha hilo akisema kuwa amekwenda nchini Hispania kumalizia kozi ya ukocha ya leseni A barani Ulaya.

“Kutokana na kutumikia adhabu ya TFF iliyotokana na mchezo dhidi ya Njombe Mji, pia tulipokea barua kutoka Bodi ya Ligi ikitutaka baada ya adhabu hiyo, asikae benchi kutokana na kuadhibiwa tena kwa kitendo cha kuonyesha kidole cha kati katika mchezo na Ruvu Shooting uliofanyika Uwanja wa Mabatini.

“Kutokana na hali hiyo ya kutokuwepo katika benchi la ufundi kwa michezo hii minne au zaidi, uongozi umemruhusu kwenda kumalizia kozi yake ya ukocha, kwani tunahofia akichelewa atapokonywa leseni,” alisema.

Father alisema kocha huyo anatarajiwa kurejea baada ya kumalizika kwa kozi hiyo, kwani mkataba wake na Azam unamalizika Julai, mwaka huu, hivyo huenda wakaanza maongezi naye ya mkataba mpya.